Shirika
la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limekiri kuwapo ubadhirifu kwenye
mkataba wa ubia na Kampuni ya Azimio Housing Estates iliyotakiwa
kuendeleza ekari 20,000 za ardhi Kigamboni na kuna hatari ya kupoteza Sh
bilioni 270.
NSSF
pia imekiri ubadhirifu katika utoaji mikopo kwenye Saccos mbalimbali
nchini ikiwamo ya Bumbuli, inayoonekana kukopeshwa zaidi ya Sh bilioni
mbili, bila kuwa na sifa huku kukiwa pia hakuna kumbukumbu ya mwaka
mzima kama walirudisha mkopo wa awali.
Mwenyekiti
wa Bodi ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe alieleza jana mbele ya Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwamba Bodi yake ilipoingia
madarakani iligundua ubovu wa mkataba huo na kusitisha kutoa fedha na
sasa inaangalia namna ya kujitoa bila kupoteza fedha zilizowekezwa.
Alisema
uwekezaji huo ambao ardhi ya mwekezaji ilipaswa kuwa ekari 20,000,
hatua ya awali ulipaswa kuanza na ekari 300, lakini uchunguzi
uliofanyika hivi karibuni ulionesha kuwa kuna ekari 3,500 pekee hali
inayoonesha udanganyifu uliofanyika tangu awali.
Pia
mwekezaji huyo alidanganya uhalisia wa bei ya ardhi hiyo, kwani
alionesha kuwa thamani ya ekari ya moja ni Sh milioni 800 wakati
kiuhalisia, ardhi hiyo thamani yake ni Sh milioni 25 peke yake.
Mwenyekiti
wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka alisema imekuwa vigumu kwa Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuthibitisha uwepo wa viwanja
hivyo kwa kukosekana hatimiliki, umiliki wa ekari 19,700 za ardhi ambazo
ni sehemu ya mtaji wa Azimio Housing Estates kwa asilimia 20, hivyo
fedha za NSSF zinakuwa kwenye hatari ya kupotea.
Alisema
NSSF ambayo inamiliki hisa ndogo kuliko Azimio, imewekeza fedha nyingi,
zaidi ya dola milioni 129 za Marekani wakati mbia huyo aliwekeza dola
milioni 5.5.
Akijibu
hoja za Mwenyekiti huyo, Profesa Wangwe alisema mradi huo ulisimama
tangu Februari kutokana na mbia kukosa fedha na kwamba hakopesheki kwani
NSSF inamdai.
Mbunge
wa Msalala, Ezekiel Maige alisema mradi huo wa Kigamboni ni mchafu na
katika mazingira hayo ambayo Bodi pia imeshituka kuwa mchafu hivyo ni
vema NSSF ingejitoa kuliko kuendelea na mkataba mbovu.
“Ni
vema ukishagundua kuwa unachezea kitenesi kichafu ambacho kilianza
kuchezewa na watu ambao wameshaondolewa, usiendelee kucheza na mtu yule
yule ili asije kukuingiza katika matatizo makubwa zaidi,” alisema Maige.
Profesa
Wangwe alisema ni vigumu kujitoa haraka kwenye mkataba huo, kutokana na
fedha nyingi waliyowekeza ambayo iko hatarini kupotea na kwamba ardhi
yote ni ya mwekezaji huyo hivyo wanatafuta namna ya kurudisha fedha
waliyowekeza hata kama haitakuwa na faida.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aesh Hilaly alihoji kama mkataba unaruhusu mwekezaji huyo kukopa ili kuendeleza mradi huo.
Mkurugenzi
wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema mwekezaji huyo alitaka kukopa
NSSF ili aendeleze mradi huo ambao umesimama lakini hakopesheki kwa
kuwa anadaiwa.
Hata
hivyo, baadhi ya wabunge walihoji uhalali wa Saccos kukopeshwa mara
mbili kwa mwaka, huku zingine zikikosa mikopo na vigezo vilivyotukia
katika kutoa mikopo hiyo.
Kuhusu
Saccos ya Bumbuli, Kaboyoka alisema mbunge wake anafahamika, hivyo
inashangaza ipewe fedha hizo kwa mwaka mmoja na kuhoji sifa zilizotumika
kuzitoa wakati Saccoss zingine hazijapata.
Alisema
ni vema ufanyike ukaguzi maalumu kwenye Saccos hiyo kwani fedha hizo ni
mafao ya wafanyakazi ingawa pia inatia shaka katika utoaji, kwani awali
Saccos hiyo ilipewa zaidi ya Sh bilioni moja na kwamba hesabu
hazioneshi, kwamba fedha hizo zilirejeshwa, lakini ndani ya mwaka mmoja
ikapewa fedha zingine.
NSSF
ilitoa mikopo kwa Saccos tisa kwa kiasi kinachozidi asilimia 50 ya
thamani ya mali za Saccos husika, kinyume na sera ya Shirika ya
kukopesha na ziliomba kiasi ambacho hazikustahili.
Katika
ripoti ya CAG mbali na Bumbuli, Saccos zingine zilizopewa fedha nyingi
ni Korongo Amcos, UMMA, SBC, Hekima, Ukombozi, Uzinza, Harbour na Umoja.
Akijibu
hoja hizo, Profesa Wangwe alisema Saccos zilizopewa fedha zaidi ya mara
mbili kwa mwaka ikiwamo ya Bumbuli iliyopewa Sh bilioni 2.473 kwa mwaka
2014/15, wakati anaingia kwenye nafasi hiyo, aliliona hilo kama tatizo
hivyo kuagiza kufanyike ukaguzi maalumu.
Alisema
waliokuwa wanasimamia Saccos hizo walisimamiswa kazi tangu Bodi mpya
ilipoingia na kwamba walisitisha kutoa mikopo ya aina yoyote katika
Saccos zote nchini, hadi uongozi wa Shirika utakapoanzisha utaratibu
mpya.
“Watu
wote waliohusika na ubadhirifu wameshaondolewa ofisini, tulishituka
kuona namna fedha hizo zilivyotolewa, si zote zilizofika kwa wahusika,
zingine ziliishia kwenye mikono ya watu, tuliona ni vema ufanyike
ukaguzi maalumu,” alisema Profesa Wangwe.
EmoticonEmoticon