Chagua Klabu inayolipa vizuri, Samatta Aambiwa na Baba yake
Habari ya Mbwana Samatta kwenda Ubelgiji bado ina utata na haijakaa
vizuri, Baba yake, Mzee Ally Samatta amemshauri mwanaye kuchagua klabu
itakayomlipa vizuri
Goal imegundua kuwa kauli hiyo ya Mzee Samatta imeibuka baada klabu mbili za Ubelgiji kuonyesha nia ya kutaka kumsajili kijana wake.
Klabu ya kwanza ni KRC Genk, ambayo kwa heshima mkataba wa awali
umesainiwa ili kumruhusu mchezaji huyo kujiunga nayo baada ya mkataba
wake na TP Mazembe kukoma ifikapo Aprili mwaka huu.
Hata hivyo mchakato huo umeonekana kukumbwa na vizuizi baada ya TP
Mazembe kuripoti kuwa imepokea ofa nzuri zaidi iliyochangamka kutoka kwa
Standard Liege ambayo imemaliza nafasi ya nne katika Ligi ya Ubelgiji.
KRC Genk ilimaliza nafasi ya saba.
Mzee Samatta akaririwa na The Citizen:
“Mimi kama baba wa mchezaji, naona ugumu katika mambo haya, lakini
shauku yangu kuu ni kuona kijana wangu akifanikiwa kama mchezaji
anayecheza Ulaya. KRC Genk imeeleza mikakati. Viongozi wake walikuja
Tanzania wakaongea na mimi na mchezaji pia. Walimfuata Mbwana hadi
Japani na akasaini mkataba wa awali. Lakini inaonekana bosi wa TP
Mazembe, Moise Katumbi hakubaliani na biashara hii, anamtaka Mbwana
kujiunga na Standard Liege badala yake.”
Aliongeza: “Siwezi kuingilia mambo yao, kwa sababu TP Mazembe ndio
waliomwezesha kijana wangu kufikia hadhi aliyo nayo sasa. Namheshimu
Katumbi kwa sababu alichangia sana mafanikio ya Mbwana. Ushauri wangu
kwake ni kuangalia klabu nzuri kwa sababu soka ni ajira”
Alieleza zaidi kuwa inaonekana kijana wake anazidi kuchanganyikiwa
kwa sababu hataki ndoto zake zizimike, ingawa bado hajalipwa kitu na
Genk, kinyume na washika dau wengine wa soka wanavyofikiri.
Mzee Samatta aliendelea: “Mwanangu ndiye muhusika mkuu katika swala
hili; yeye ndiye mwenye uamuzi wa mwisho ni wapi anataka kwenda, ingawa
natambua kwamba kuna faida nyingi za kujiunga na Genk kutokana na
historia yake. Waafrika wengi wamefanikiwa kucheza kwenye timu za klabu
kubwa Ulaya, hasa Uingereza wakitokea klabu hiyo.
“Ni pamoja na Thibaut Courtois na Kevin De Bruyne waliojiunga na
Chelsea na Christian Benteke ambaye alijiunga na Aston Villa na sasa
anacheza Liverpool.”